Wananchi Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro wameshauriwa kuacha kilimo cha mazoea na badala yake wawe na mtazamo chanya wa kulima mazao yanayoendana na soko la sasa kama parachichi.
Kauli hiyo inakuja baada ya zao la tangawizi linalolimwa kwa wingi zaidi Wilayani Same kuonekana kushuka bei na kusababisha hasara kwa wakulima wa zao hilo ambalo gharama yake ya uzalishaji ni kubwa ukilinganisha na mazao mengine.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Mhe.Yusto Mapande wakati akizungumza katika Kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Mei 5,2023.
Mwenyekiti alishauri wananchi hao kulima zao la parachichi kwani maeneo ambayo tangawizi ilikuwa ikilimwa ni maeneo yanayoweza kurutubisha pia zao la parachichi ambalo kwa sasa linafanya vizuri sokoni.
“Same tunataka tuwe na mazao mawili ya kimkakakti ambayo ni parachichi za muda mfupi kwa maeneo ya milimani na zao la mkonge kwa wananchi wa ukanda wa tambarare” amesema Mhe.Mapande.
Akichangia hoja hiyo Diwani wa Kata ya Ruvu Yaigongo Mrutu amesema parachichi ni zao lenye soko kubwa ndani na nje ya nchi hivyo wamelibeba kama zao la kimkakati kwa hiyo wataendelea kuhamasisha wananchi kuwekeza kwenye kilimo cha mazao hayo.
Wamesema uwepo wa zao hilo utatatua changamoto kubwa ya anguko la bei kwenye zao la tangawizi ambalo kwasasa halina soko na bei yake kuwa chini na wakulima kutumia muda mrefu kulihudumia lakini hawapati faida kwani awali tangawizi ilikuwa inauzwa Tsh.3,000/- kwa kilo lakini kwasaa imeshuka hadi Tsh.400 kwa kilo.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same,Anastazia Tutuba amesema tayari Kata ya Chome Wilayani humo imeshaanzisha vitalu vya parachichi zinazokomaa muda mfupi na kushauri wananchi wengine kupata miche kutoka Chome wakati Halmashauri ikihamasisha Kata nyingine kuanzisha vitalu vya miche.
“Kwa upande wa uhamasishaji wa kilimo cha katani tayari tumetenga ekari 3,000 katika Kata ya Makanya na wawekezaji wameshapatikana hivyo tunatarajia eneo lile ndio liwe la mfano kwa kilimo cha Mkonge”Amesema Tutuba.
The Way Through Mkomazi Nationa Park or District Hospital(Kibacha Rd)
Sanduku La Posta: P.O.Box 138
Simu ya mezani: +255 27 2758034
Simu Ya Mkononi: +255 717657681
Email: ded@samedc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.