Naibu Katibu Mkuu (Afya) Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Wilson Mahera ameahidi kuipatia Wilaya ya Same magari matatu ya Idara ya Afya ili kurahisisha kazi mbalimbali zinazofanywa na Idara hiyo katika Wilaya ya Same.
Dkt.Mahera ameyasema hayo akiwa katika ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa hospitali mpya ya Wilaya ya Same ambapo alisema magari yatakayotolewa kuwa ni magari mawili ya kubebea wagonjwa (ambulance) pamoja na gari moja ya matumizi ya kawaida (hardtop).
"Utaratibu wa kupatiwa gari mbili yaani ambulance moja na hardtop moja umeshakamilika na mtazipokea wakati wowote lakini ambulance moja mtasubiri kidogo"alisema Dkt.Mahera
Pia Naibu Katibu Mkuu huyo ameahidi kuiongezea Hospitali hiyo fedha kwaajili ya kumalizia awamu ya pili ya mradi huo ambayo inajumuisha ujenzi wa Jengo la Utawala,Jengo la Kufulia,Wodi za Wagonjwa .
“Niwapongeze kwa kuanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje (OPD) katika Hospitali hii lakini niwaahidi kuwa tutaleta fedha za ukamilishaji wa Mradi huu ili majengo yote yaweze kutoa huduma na Mradi huu uweze kuwa na tija kwa wananchi” alisema.
Akitoa taarifa ya Ujenzi huo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same Dkt. Alex Alexander alimuomba Naibu Katibu Mkuu kuipatia Hospitali hiyo pamoja na Wilaya nyongeza ya Watumishi kwani Wilaya inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi wa Afya.
Aidha Dkt. Alex aliiomba Serikali kusaidia kujenga nyumba za Watumishi kwenye hospitali hiyo ya Wilaya kwani hakuna nyumba za kupanga karibu na eneo la Hospitali.
"Tunakabiliwa pia na changamoto ya ukosefu wa uzio kwaajili ya usalama kwasababu hapa ni mapitio ya Tembo hivyo tunahitaji uzio kwaajili ya usalama wa Watumishi na Wagonjwa”alisema Dkt Alex.
Naibu Katibu Mkuu Dkt Mahera alisema Serikali inatarajia kuajiri watumishi wapya wa sekta ya Afya mwezi huu (Novemba 2023) hivyo Wilaya ya Same itapata mgawo.
Aidha Dkt. Mahera alisema katika kukabiliana na Upungufu mkubwa wa watumishi wa Afya hapa nchini Serikali inatarajia kuajiri wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao ni wahitimu wa kidato cha nne ambao watapatiwa mafunzo ya miezi sita ili waweze kusaidia kutoa huduma za afya kwa kushirikiana na madaktari na wauguzi waliopo.
The Way Through Mkomazi Nationa Park or District Hospital(Kibacha Rd)
Sanduku La Posta: P.O.Box 138
Simu ya mezani: +255 27 2758034
Simu Ya Mkononi: +255 717657681
Email: ded@samedc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.